MKUU wa Wilaya ya Songea Mheshimiwa Wilman Kapenjama Ndile amewataka watumishi wa umma kufanya kazi kwa ushirikiano na umakini ili ziweze kuleta matokeo chanya katika Halmashauri.
Ameyasema hayo wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea alipokuja kujitambulisha katika ukumbi wa mikutano Lundusi-Peramiho ikiwa ni mara ya kwanza tangu alipoteuliwa na Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan Januari 25, 2023.
“Napenda kuchukua nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuniamini na kuniteua kuwatumikia wananchi wa Wilaya ya Songea nawaahidi kuwapa ushirikiano wa hali ya juu katika kuhakikisha kila mmoja anatekeleza majukumu yake vizuri”, amesema Mheshimiwa Ndile.
Aidha, amewasisitiza Viongozi wa Kata na Vijiji wakishirikiana na walimu wakuu kufanya ufuatiliaji kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza ambao hawajaripoti shule wahakikishe wazazi wanapeleka watoto hao shule kabla hawajachukuliwa hatua za kisheria.
Akizungumza katika kikao iko amekemea uingizaji holela wa mifugo katika vijiji kwani Wilaya ya Songea ni ya kilimo na sio ufugaji hivyo ameahidi kulisimamia vyema swala hili la uingizaji wa mifugo.
Mheshimiwa Ndile ameupongeza uongozi wa Halmashauri kwa usimamizi mzuri wa miradi na swala zima la ukusanyaji wa mapato.
Kwaupande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea Mheshimiwa Menas Komba akizungumza kwa niaba ya watumishi wote amemkaribisha Mheshimiwa Ndile, pia amemuahidi kumpa ushirikiano wa kutosha katika kutekeleza majukumu.
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa