Waziri wa Mifugo na Uvuvi Luhaga Mpina amewaagiza viongozi wa Mkoa wa Ruvuma kufanya utaratibu wa kujenga hosteli na kiwanda cha kutengeneza chakula cha samaki katika kituo cha kuzalishia samaki Luhira kilichopo Manispaa ya Songea.
Amesema hosteli hiyo itasaidia kutoa mafunzo ya muda mfupi na kuwatunuku vyeti wahitimu mara baada ya kumaliza mafunzo na kiwanda kitasaidia kuzalisha chakula cha samaki hivyo uzalishaji wa samaki utaongezeka.
Waziri Mpina ameyasema hayo alipofanya ziara ya kikazi katika Mkoa wa Ruvuma ,mara baada ya kutembelea kituo hicho ambacho pia kinahusuka na masuala ya utalii.
Mpina amepongeza kazi nzuri inayofanywa na kituo hicho na kuagiza mafanikio yanayopatikana yaweze kutoa fursa mbalimbali ikiwemo mafunzo na kupata elimu ambayo itawasaidia kuboresha kipato na kuinua uchumi.
“Nimefurahishwa na kituo hiki ambacho ni cha mfano Tanzania,naagiza mjitangaza kwa wananchi ili watu waweze kujipangia ratiba ya kuja kujifunza hapa bila kuathiri shughuli zao za kijamii’’,amesisitiza.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Songea pololet Mgema amesema kituo cha kuzalishia vifaranga vya samaki Luhira kimekuwa kituo cha kiutalii na kwamba likiboreshwa ni chanzo cha mapato.
Luka Mgwena ni Afisa Mfawidhi wa Kituo cha samaki Luhira amesema kituo hicho kina uwezo wa kuzalisha vifaranga 40,000 kwa wiki na kina uwezo wa kusambaza ndani ya Mkoa na nje ya Mkoa ambapo tayari kituo kimesambaza vifaranga,Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali katika Mkoa wa Mbeya,Mkoa wa Songwe na Njombe.
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa