Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Hussein Bashe, amefanya ziara ya kukagua vituo vya ununuzi wa mahindi katika Halmashauri ya Wilaya ya Songea, akiridhishwa na utaratibu uliowekwa na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) wa kununua mahindi bora.
Mhe Hussein Bashe, ameendelea na jitihada zake za kuboresha sekta ya kilimo nchini kwa kufanya ziara ya ukaguzi katika vituo viwili vya ununuzi wa mahindi, Kizuka na Mgazini. Ziara hiyo imelenga kukagua utaratibu wa ununuzi wa mahindi katika vituo hivyo, ambapo aliridhishwa na hatua zinazochukuliwa na NFRA za kuhakikisha ununuzi wa mahindi yaliyochaguliwa kwa umakini.
Waziri Bashe, akizungumza na wakulima, aliahidi kuwa serikali itaongeza maghala ya kuhifadhia mazao ili kupunguza changamoto ya uhaba wa nafasi ya kuhifadhi mazao baada ya kuvuna. Aidha, alieleza mpango wa serikali wa kuboresha miundombinu ya usafiri, hususan barabara zinazoelekea vituo vya kuuza mazao, jambo ambalo litasaidia kupunguza gharama za usafirishaji kwa wakulima.
Katika hatua nyingine, Waziri Bashe alitoa ahadi ya kuweka mashine za kisasa za kuchambua mahindi katika msimu ujao wa kilimo. Alieleza kuwa mashine hizo zitapunguza muda wa kuchambua mahindi, tofauti na sasa ambapo wakulima wanatumia machekeche yanayochambua gunia moja kwa siku. Alisema, "Lengo ni kuhakikisha kwamba wakulima wanatumia muda mfupi kufanya kazi, hivyo mashine hizi zitasaidia sana katika kuboresha uzalishaji."
Waziri Bashe pia alizungumzia changamoto ya mbegu feki, akiahidi kuwa msimu ujao wakulima hawatouziwa mbegu zisizo na ubora. Alifafanua kuwa serikali itaimarisha udhibiti wa mbegu zinazouzwa madukani kwa kuweka mfumo wa kidijitali utakaowezesha wakulima kuhakiki ubora wa mbegu kabla ya kununua. "Tumechunguza na kugundua kuwa moja ya sababu za mahindi machafu ni kutokana na mbegu feki. Kwa hiyo, tutahakikisha mfuko wa mbegu unakuwa na 'barcode' ambapo mkulima ataweza kuingiza namba kwenye simu na kupata taarifa ikiwa mbegu ni feki au halali," aliongeza Waziri.
Wananchi wa Kizuka na Kilagano walimshukuru sana Waziri Bashe kwa kuwatembelea na kujionea changamoto wanazokabiliana nazo. Walitoa wito kwa serikali kuzifanyia kazi changamoto hizo ili kuboresha uzalishaji na kuleta tija kwa wakulima wa maeneo hayo.
Ziara ya Waziri Bashe ni sehemu ya juhudi za serikali kuboresha sekta ya kilimo, ambayo ni uti wa mgongo wa uchumi wa taifa, na kuhakikisha kuwa wakulima wanapata mazingira bora ya kuzalisha mazao kwa tija zaidi.
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa