Leo Oktoba 1, 2025 Timu ya wataalamu kutoka Idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ya Halmashauri ya Wilaya ya Songea, ikiongozwa na Ndugu Godson Msalilwa, imeendelea na ziara ya kukagua na kutoa elimu kwa wakulima wa zao la parachichi katika Kata ya Peramiho.
Katika ziara hiyo, Ndugu Msalilwa aliwapongeza wakulima kwa kujitolea na kuwekeza katika zao hilo, akibainisha kuwa parachichi ni moja ya mazao ya kimkakati ambayo Halmashauri imepanga kuyawekea mkazo kutokana na faida zake za kiuchumi na uendelevu. Aliongeza kuwa parachichi ni zao la kudumu linaloweza kuwainua wakulima kiuchumi ukilinganisha na mahindi ambayo kwa muda mrefu yamekuwa tegemeo kubwa la wakulima wengi.
"Tunawapongeza kwa kuwa wakulima wa mfano mliothubutu kuwekeza kwenye parachichi. Zao hili lina tija kubwa na litasaidia kuinua kipato cha kaya zenu endapo mkizingatia kanuni bora za kilimo," alisema Msalilwa.
Aidha, aliwaelekeza wakulima hao kuzingatia mambo matatu muhimu ili kupata mazao bora ya parachichi, ambayo ni: usafi wa shamba, matumizi ya mboji au samadi, pamoja na kuhakikisha uwepo wa maji ya kutosha kipindi cha masika na kiangazi.

Kwa upande wake, Afisa Kilimo wa Halmashauri hiyo, Frank Sungau, aliwasisitiza wakulima kutumia dawa za kuua wadudu waharibifu na mbolea kwa wakati unaotakiwa, ili kuongeza tija na ubora wa mazao yao.
Mmoja wa wakulima hao, Ndugu Lukasi Kauli, alitoa shukrani kwa wataalamu wa kilimo kwa kuwapelekea elimu hiyo, akisema imekuwa msaada mkubwa kwao kwani walikuwa wakikumbana na changamoto ya wadudu waharibifu bila ufumbuzi wa kitaalamu.
"Tumefurahi kupata elimu hii, hasa kuhusu matumizi sahihi ya dawa za kuua wadudu. Changamoto hii ilikuwa inatukwamisha kwa muda mrefu, lakini sasa tunaamini mavuno yetu yatakuwa bora," alisema Kauli.
Ziara hiyo ni mwendelezo wa juhudi za Halmashauri ya Wilaya ya Songea katika kuwajengea uwezo wakulima wake ili kuendeleza kilimo chenye tija na kuongeza mapato ya kaya pamoja na pato la Halmashauri.
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa