Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Mhe Stephen Wasira, leo Juni12, 2025 amefika Halmashauri ya Wilaya ya Songea na kukutana na viongozi mbalimbali ikiwemo wanachama wa CCM na kuwapongeza kwa mafanikio makubwa ya ukamilishaji wa miradi ya maendeleo.
Mkutano huo ulifanyika katika ukumbi wa Jenista Mhagama uliopo katika Shule ya Sekondari Maposeni, Halmashauri ya Wilaya ya Songea.
Akitaja mafanikio hayo, Mhe. Wasira alisema "Katika kipindi cha miaka minne tu, ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Songea, Mheshimiwa Rais amejenga shule mpya nne za sekondari, madarasa mapya 142, zahanati 17, vituo vya afya vinne, na pia umeme umefika katika vijiji vyote vya halmashauri hii."
Katika hotuba yake, Wasira amempongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi kubwa anazoendelea kuzifanya katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa wananchi, akisema kuwa hiyo ndiyo dhana ya msingi ya Ilani ya CCM.
Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas Ahmed, alimshukuru Makamu Mwenyekiti CCM Taifa kwa kufanya ziara Mkoani humo, hususan katika Halmashauri ya Wilaya ya Songea, pia alituma salamu za Shukrani kwa Mhe Rais kwa miradi mingi iliyofika Mkoani Ruvuma.
"Ujio wako ni wa kipekee. Ninashukuru kwa ushirikiano mkubwa ninaoupata kutoka Chama Cha Mapinduzi katika kutekeleza majukumu yangu kwa wananchi," alisema Kanali Ahmed.
Alimpongeza Mbunge wa Jimbo la Peramiho, Mheshimiwa Jenista Mhagama, kwa kazi nzuri anayoifanya. "Mheshimiwa Jenista amekuwa akilitumikia Jimbo la Peramiho kwa moyo wa kujituma. Kila eneo alilopewa kulitumikia amelitendea haki inayostahili, na mchango wake unahisiwa ndani na nje ya mkoa huu," aliongeza.
Aidha, Ndugu Wasira aliwataka wajumbe wote walioshiriki mkutano huo kuwa mabalozi wa kudumisha na kulinda amani ya taifa, hususan katika kipindi hiki ambacho nchi inaelekea kwenye Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba 2025. "Ni wajibu wa kila mwananchi kuhakikisha kuwa tunalinda misingi ya amani na mshikamano wa kitaifa. Amani ni msingi wa maendeleo yetu," alisisitiza.
Katika hatua nyingine, Wasira alitoa shukrani za dhati kwa wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea kwa zawadi walizompatia. Zawadi hizo ni pamoja na fedha taslimu shilingi 150,000, mbuzi mmoja, jogoo mmoja, mahindi kilo 500, mpunga kilo 200 na maharagwe kilo 110 ambazo ziliwasilishwa kwake na Katibu Tawala wa Wilaya Ndg. Mtela Mwampamba.
Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama na Serikali, pamoja na wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya Halmashauri ya Wilaya ya Songea.
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa