Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea, Bi Elizabeth Mathias Gumbo, ametoa wito kwa wasimamizi wa miradi ya maendeleo kuhakikisha usimamizi makini na wenye tija katika utekelezaji wa miradi inayotarajiwa kuanza hivi karibuni, yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 1.6.
Akizungumza katika kikao kazi kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri hiyo, Gumbo aliwataka wasimamizi hao kufuata kikamilifu maelekezo waliyopewa, ikiwa ni pamoja na kuzingatia ushirikishwaji wa kamati za ujenzi katika kila hatua ya utekelezaji pamoja na kufanya manunuzi kwa kutumia Mfumo wa Kitaifa wa Manunuzi kwa Njia ya Kielektroniki (NeST).
"Ni muhimu kuhakikisha miradi hii inatekelezwa kwa kuzingatia thamani ya fedha na kwa uwazi mkubwa, ili wananchi wapate huduma bora na ya kudumu," alisema Gumbo.
Kwa upande wake, Afisa Mipango wa Halmashauri hiyo, Ndugu Exavery Luyagaza, alipokea maelekezo hayo kwa niaba ya timu ya wasimamizi wa miradi na akaahidi kuyasimamia kikamilifu ili kuhakikisha utekelezaji wa miradi unaendana na viwango vilivyowekwa, na kwamba kila hatua itasimamiwa kwa uwazi na uadilifu.
Aidha Mhandisi wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea, Bi. Flora Tairo, aliwataka wasimamizi hao kuzingatia makadirio ya ujenzi (BOQ) ili kupata majengo yenye ubora unaostahili na kuzuia upotevu wa rasilimali.
“Miradi yote itekelezwe kulingana na BOQ, ili tufikie viwango vya kitaalamu na kuepuka hasara zisizo za lazima,” alisisitiza Mhandisi Tairo.
Miradi inayotarajiwa kutekelezwa ni pamoja na Umaliziaji wa vyumba vya madarasa katika Shule ya Msingi Ndirima, Umaliziaji wa maabara katika shule za sekondari za Darajambili, Lupunga na Mhalule, Ujenzi wa madarasa na vyoo katika shule za msingi Magagura na Namakinga, Ujenzi wa vituo vya afya katika kata za Mpandangindo na Peramiho, Umaliziaji wa zahanati katika vijiji vya Morogoro, Magima na Ndongosi, Umaliziaji wa vituo vya afya katika kata za Kilagano, Magagura na Matimila.
Utekelezaji wa miradi hii unatarajiwa kuongeza upatikanaji wa huduma bora za elimu na afya kwa wananchi wa Wilaya ya Songea, na hivyo kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa