WANANCHI wa Kata ya Litisha waanza kunufaika na mradi wa maji
Wanachi wa Kata ya Litisha Wilayani Songea Mkoani Ruvuma wameanza kunufaika na huduma ya mradi wa maji, mradi ulioanza kutekelezwa mwezi Mei 29 ,2020 na utakamilika Juni 30,2021
Mkurugenzi wa Mamlaka ya maji taka na usafi wa mazingira Ruvuma Mhandisi Patrick Kibasa amesema mradi wa maji katika Kijiji cha Litisha ulisanifiwa kwa gharama ya zaidi ya shilingi milioni 473,mpaka sasa mradi huo umekamilika kwa asilimia 70 .
Mhandisi Kibasa amesema ujenzi wa mradi huo ni wa kisima chenye urefu wa mita 181 na kina uwezo wa kuzalisha maji lita 9,000 kwa saa ambapo amesema kukamilika kwa mradi huo kutawanufaisha wakazi 3,226 sanjari na kuokoa muda wa wananchi ambao walikuwa wakiutumia kufuata huduma hiyo umbali mrefu.
Ameitaja miradi mingine ya maji itajengwa katika Vijiji vya Litowa,Peramiho (B) na Nakahuga kupitia mfuko wa maji wa Taifa.
Naye Mwenyekiti wa Kijiji Litisha Saidi Hashimu kwa niaba ya wananchi ameishukuru Serikali kwa kuwajengea mradi huo na kutatua changamoto maji wakabili ikiwemo maji ambayo yatawasaidia kuongeza shughuli za kiuchumi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati ya siasa Mkoa wa Ruvuma Oddo Mwisho ametoa wito kwa wananchi kuacha kuhujumu miundo mbinu ya maji kwa makusudi kwani kitendo hicho kinawakosesha wananchi kupata huduma ya maji kwa uzembe wa watu wachache au mtu mmoja.
Mwisho ametoa rai kwa wananchi kulinda vyanzo vya maji ,badala yake walinde vyanzo hivyo kupanda miti rafiki ya maji ambayo itasaidia vyanzo hivyo kuwa endelevu na huduma ya maji kupatikana kwa muda wote.
Mjumbe wa Kamati hiyo ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme amesema hatamfumbia macho mtu yoyote atakayethubutu kuharibu na kuhujumu miundo mbinu ya maji kwa sababu Serikali inatoa fedha nyingi kwa ajili ya kujenga miradi ya maji,hivyo lazima miradi hiyo ilindwe na kutunzwa.
“Serikali itahakikisha mazingira na vyanzo vya maji vinatunzwa”,amesisitiza Mndeme
Kamati ya Siasa ya CCM mkoa wa Ruvuma imemaliza ziara ya siku tatu kukagua miradi ya maji katika wilaya za Songea na Namtumbo.
Imeandaliw na kuandikwa na
Jacquelen Clavery
Afisa Habari Songea DC
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa