WANAFUNZI wa shule ya Sekondari Mpitimbi wameishukuru Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Songea kwa kuwajengea bweni jipya na la kisasa lililowatengenezea mazingira mazuri ya kujisomea.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wameipongeza na kuishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Mbunge wa Jimbo la Peramiho Mheshimiwa Jenista Joakim Mhagama kwa jitihada za kuboresha miundombinu ikiwemo ujenzi wa bweni na vyumba viwili vya madarasa vilivyojengwa kwa fedha za mpango wa maendeleo kwa ustawi wa jamii na mapambano dhidi ya UVIKO-19.
Akizungumza Mwalimu wa ujenzi Mathew Haule amesema, Shule ilipokea jumla ya shilingi Milioni 80 kutoka Serikalini kwaajili ya ujenzi wa bweni ambapo fedha zilizotumika ni shilingi 79,995,561 na kubaki shilingi 4,400.
Mwalimu Haule amesema hatua ya Serikali kujenga bweni kwaajili ya wanafunzi wa kike imesaidia wanafunzi kuishi kwenye mazingira mazuri ya kujisomea muda wa ziada pamoja na kuwaongezea ulinzi watoto wa kike.
Kwaupande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea Ndugu Neema Maghembe amesema kuwa kwa mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali imetumia jumla ya shilingi Milioni 480 kwaajili ya kujenga mabweni sita katika shule za Sekondari.
Aidha ameongeza kuwa kwa mwaka 2022/2023 Serikali imepanga kutumia Shilingi Milioni 320 kwaajili ya kujenga mabweni mengine manne ambapo wameshapokea Shilingi Milioni 160 kati ya Shilingi 320 kwaajili ya kujenga mabweni mawili.
‘’Napenda kutoa shukrani za dhati kwa Serikali yetu ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan, na Mbunge wa Jimbo la Peramiho Mhe.Jenista Joakim Mhagama kwa kuendelea kuikumbuka Halmashauri kwa kutuletea fedha kwaajili ya kutekeleza miradi na kuboresha huduma mbalimbali za kijamii’’, amesema Ndugu Neema.
Pia ametoa shukrani kwa baraza la Madiwani wakiongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri Mhe.Menas Komba, Viongozi wa Chama pamoja na timu ya wataalamu kwa kushirikiana vyema katika kutekeleza na kuisimamia miradi.
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa