Kamati ya Lishe Halmashauri ya Wilaya ya Songea leo Octoba 25, 2023 imefanya Kikao cha Kujadili taarifa za utekelezaji wa hatua za mikataba ya lishe kwa kipindi cha Robo ya kwanza kuanzia Julai hadi Septemba 2023.
Akifungua kikao Mkuu wa Wilaya ya Songea Mhe. Wilman Kapenjama Ndile amewata wakuu wa shule waanzishe miradi ya migahawa shuleni ili iweze kuhudumia wanafunzi vitafunwa na mbogamboga kwa manufaa ya afya za wanafunzi.
“Wakuu wa shule wawasiliane na Mkuu wa Shule ya Sekondari Songea Girls ili waweze kujua wao wamefanyaje hadi wameweza kuanzisha mgahawa wa shule ambao unawahudumia wanafunzi, tusiamini sana vyakula vinavyopikwa nje ya shule wanavyouziwa Wanafunzi wetu hii itasaidia kulinda afya za wanafunzi pia ni njia ya kuingiza mapato katika Shule”, amesema Mhe. Ndile
Aidha, Mhe. Ndile amewataka Watendaji wa Kata kwa kushirikiana na Walimu mashuleni kuanzisha kilimo cha mbogamboga na matunda ambazo zitasaidia wanafunzi kula mlo kamili pindi wanapokuwa shuleni.
Kwa upande wake Afisa Lishe wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea Bi. Joyce Kamanga amesema “Kwa upande wa Divisheni ya Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii tumeendelea kutekeleza hatua za Lishe kwa asilimia 100% huku tukifanikiwa kutoa elimu kwa wananchi wa Kata zilizopo katika Halmashauri kuhusu masuala ya lishe bora, pia kuhakikisha kila kijiji kinaadhimisha siku ya Afya na Lishe ambapo Watumishi wa Afya wanatoa Elimu juu ya matumizi bora ya lishe kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano na Wamama Wajawazito”.
Mwisho katika kikao hicho wajumbe walikubaliana katika kuongeza jitihada zaidi kuhamasisha na kutoa elimu kwa wananchi juu ya masuala ya lishe ili kuboresha afya na kulinda afya zao.
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa