Wakulima Halmashauri ya Wilaya ya Songea, wamehimizwa kuzingatia mbinu bora za uvunaji wa mahindi ili kupunguza upotevu wa mazao na kuhakikisha ubora wa mavuno unadumu hadi sokoni.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea Ndugu Frank Sungau, ambaye amekaimu Idara hiyo, Amesema mahindi yanapaswa kuvunwa yakiwa yamekomaa vizuri na kukauka kwa kiwango kinachotakiwa, huku dalili kuu za kukomaa zikiwa ni magunzi kuanza kuinama chini na majani ya mabua kukauka.
“Ni muhimu kuvuna mahindi mapema baada ya kukomaa ili kupunguza hasara inayoweza kutokea kutokana na kuchelewa kuvuna, hasa kipindi hiki ambacho hali ya hewa inaweza kubadilika ghafla,” alieleza Sungau.
Aidha, aliwaonya wakulima dhidi ya uuzaji holela wa mahindi kwa kushindwa kuzingatia mahitaji ya chakula kwa familia zao kwa mwaka mzima. “Kila kaya izingatie idadi ya wanachama wake, hakikishe kuna chakula cha kutosha kwa matumizi ya mwaka mzima ndipo ziada iuzwe,” alisisitiza.
Wakati huo huo, Sungau amesema kuwa Serikali imepanga kuanza rasmi ununuzi wa mahindi kwa msimu wa mwaka 2025/2026 kuanzia Julai 1, 2025 kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Kanda ya Songea.
Katika hatua nyingine, Halmashauri ya Wilaya ya Songea imeendelea kushika nafasi ya kwanza kwa uzalishaji wa mahindi Mkoani Ruvuma kwa zaidi ya misimu mitano mfululizo, na hivyo kuchangia Mkoa wa Ruvuma kuongoza kitaifa katika uzalishaji wa mazao ya chakula kwa zaidi ya miaka mitano.
“Ushirikiano wa karibu kati ya maafisa ugani na wakulima, pamoja na jitihada za Serikali katika kuwapatia pembejeo za ruzuku, ndiyo msingi wa mafanikio haya,” alisema Sungau.
Ameeleza kuwa Serikali imekuwa ikiwezesha wakulima kwa kuwapatia mbolea na mbegu bora kwa njia ya ruzuku, pamoja na kuwapatia maafisa ugani vitendea kazi kama pikipiki na vifaa vya kupimia udongo ili kuongeza ufanisi.
Kwa msimu ujao wa kilimo, mkakati uliowekwa ni kuongeza tija ya uzalishaji kwa kupitia mafunzo ya maafisa ugani walioko katika kata na vijiji, kupanua ukubwa wa mashamba, na kuongeza mavuno kutoka tani nne hadi tani tano kwa hekta moja.
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa