KATIBU Tawala Wilaya ya Songea Ndugu Pendo Daniel ambaye amemwakilisha Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Peramiho Mheshimiwa Jenista Joakim Mhagama amefanya uzinduzi wa maadhimisho ya siku ya mwanamke duniani ambayo yamefanyika Katika Kata ya Parangu Halmashauri ya Wilaya ya Songea.
Akizungumza katika uzinduzi huo amewataka wananchi kubadilika na kuondoa fikra potofu kwamba mwanamke au mtoto wa kike hana uwezo wa kufanya shughuli zozote za maendeleo kama kupata Elimu na kupata nafasi ya kutoa maamuzi hivyo amesema jinsia zote ni sawa katika kuleta maendeleo endelevu katika Taifa.
Ndugu Pendo ametoa wito kwa jamii kupeleka watoto shule bila kubagua kwani watoto wakipata Elimu itawasaidia kutimiza ndoto zao.
Pia amewasisitiza wataalamu kuendelea kutoa elimu ya kijinsia katika taasisi mbalimbali kwani watoto watakuwa na uelewa juu ya kupata haki zao za Msingi.
" Nachukua nafasi hii kutoa pongezi Kwa wataalamu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Kwa kupita mashuleni na kutoa elimu ya kijinsia hii itawasaidia wanafunzi na watu wengine kujua kuwa jinsia zote zipo sawa hivyo basi hakutakiwi kuwa na tofauti zozote kati ya mwanamke na mwanaume", amesema Ndugu Pendo.
Vilevile Ndugu Pendo amewasisitiza Wanawake Viongozi kutumia vizuri nafasi walizopewa katika utendaji kazi ili kuleta maendeleo Kwa jamii anayoiongoza.
Amesema ni wajibu wa Kila mtu kuelimisha,kukemea na kuchukua hatua Kwa watu wanaofanya matendo maovu ambayo yanasababisha watoto wa kike wasiweze kufikia malengo yao.
Kwaupande wake Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya Bi Zawadi Nyoni ameeleza maudhui ya siku ya Wanawake duniani amesema mikakati iliyowekwa na Serikali ni kuhakikisha Wanaume na Wanawake wanajengewa uwezo kuhusu maswala ya jinsia na uwezeshaji wa Wanawake katika mafunzo mbalimbali.
Ameongeza kuwa Serikali imedhamiria kuongeza ushiriki wa Wanawake katika kuongeza uzalishaji wa bidhaa na kuzifikisha kwenye masoko ya ndani na nje kwa lengo la kujenga taifa linalojitegemea.
Kauli mbiu "Ubunifu na mabadiliko ya teknolojia chachu katika kuleta usawa wa kijinsia".
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa