Mkuu wa Wilaya ya Songea Ndugu Pololet Mgema amezindua jukwaa la Wanawake wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea na kuwataka kutumia jukwaa hilo kwa ajili ya kujadili fursa na changamoto zinazowakabili katika kujiletea maendeleo.
Akimkaribisha mkuu wa Wilaya ya Songea Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ndugu Simon Bulenganija amesema Jukwaa la wanawake ni muhimu kwa Ustawi na maendeleo ya jamii nzima kwani ukimkomboa mwanamke kiuchumi umekomboa jamii nzima.
Afisa maendeleo ya jamii wa wilaya bi, Judith Ngowi amesema uwezeshaji wa wanawake kiuchumi unasimamiwa kikamilifu na kamati zimeundwa kuanzia ngazi ya Taifa mpaka kijiji na pia kuna waratibu wa dawati la uwezeshaji wa wananchi kiuchumi kuanzia ngazi ya Taifa hadi Kata. Kauli mbiu ya mwaka huu ni ‘’Wezesha wanawake kiuchumi ili kujenga uchumi wa kati na Tanzania ya viwanda’’
Uanzishwaji wa jukwaa la kuwawezesha wanawake ni agizo la Mh. Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan, ambaye aliteuliwa na katibu mkuu wa umoja wa mataifa kuwa Mjumbe mmojawapo wa timu ya viongozi na wataalamu ambao watafanya kazi kama chombo cha juu katika kupunguza na kuondoa pengo kubwa ambalo limejengeka Duniani na kuongeza ushiriki wa wanawake katika uchumi Duniani na kote ili kufikia maendeleo ambayo pia yamesisitiza uwezeshaji wa Wanawake Kiuchumi.
Lengo kuu la jukwaa la uwezeshaji Wanawake kiuchumi ni kukutana pamoja na kujadili fursa, Changamoto na jinsi ya kushiriki kikamilifu katika biashara na shughuli nyingine za kiuchumi katika Wilaya.
Vilevile kuongeza uelewa wa Wanawake katika upatikanaji wa wa Mitaji, Sheria za nchi katika masuala ya uchumi na jinsi ya kujitegemea kiuchumi. Kwani imebainika kuwa Wanawake hawapati fursa za kutosha za kiuchumi hapa Tanzania na duniani kote. Hii inatokana na kuto kuwa na usawa katika fursa, uwezo wa kupata mitaji na ajira.
Hivyo Jukwaa hili litasaidia kuondoa matabaka na sheria kandamizi za uchumi kwa Wanawake katika kuleta maendeleo ya usawa katika pato la familia, jamii na Taifa kwa ujumla.
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa