WANANCHI Halmashauri ya Wilaya ya Songea wametakiwa kuendelea kuchanja chanjo ya POLIO na UVIKO-19 ili kuweza kupunguza makali ya magonjwa hayo.
Hayo ameyasema Mkuu wa Wilaya ya Songea Mheshimiwa Pololet Kamando Mgema katika kikao cha utekelezaji wa tathmini ya kamati ya afya msingi katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea Lundusi Peramiho.
Amesema kutoka Agosti 2021 hadi kufikia Agosti 2022 Halmashauri imefanikiwa kutoa chanjo ya UVIKO-19 kwa watu 100,842 sawa na asilimia 110.23 hivyo imeweza kuvuka lengo la asilimia 70 iliyotakiwa.
Pia amesema kutoka mwezi Machi 2022 hadi tarehe 05 Septemba 2022 Halmashauri imeweza kuwafikia watoto 37,205 sawa na asilimia 124.3 ya lengo la watoto 29,928.
‘’Hatuna budi kujipongeza kwa matokeo makubwa ambayo tumeyapata kuwakinga watoto wetu juu ya ugonjwa wa POLIO Na kuikinga jamii kwa ujumla juu ya ugonjwa wa UVIKO-19, hivyo Halmashauri yetu imeweza kuvuka lengo la asilimia iliyotakiwa kwa chanjo zote’’, amesisitiza DC Mgema.
Kwaupande wake Mratibu wa chanjo Osmunda Paul amesema ugonjwa wa POLIO unaweza ukakingwa kwa kupata chanjo lakini hauna tiba hivyo mtu akipata ugonjwa huo unasababisha ulemavu wa moja kwa moja.
Ametoa rai kwa viongozi kuendelea kuwahamasisha wazazi kupeleka watoto katika vituo vya kutolea huduma ya afya ili kupatiwa chanjo ili wawakinge na ugonjwa huu hatari.
POLIO ni ugonjwa ambao unasababishwa na virusi vya POLIO baada ya kuingia mwilini unaathiri mfumo wa fahamu, ugonjwa huu unaweza kumpata mtu kwa kunywa au kwa kula chakula ambacho kina virusi au vimelea vya ugonjwa huu.
Imeandaliwa na Bahati Nyoni.
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini.
09 Septemba 2022.
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa