Wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea, wanategemea kunufaika na ujenzi mpya wa Mradi wa Barabara ya Likuyufusi hadi Mkenda unaitarajia kuanza hivi karibuni
Akizungumza na wanachi wa Jimbo la peramiho, Mbunge wa Jimbo la Peramiho ambaye pia ni Waziri wa Afya, Mhe Jenista Mhagama, amesema mradi wa ujenzi wa barabara ya Likuyufusi–Mkenda utaleta mageuzi makubwa katika sekta ya usafirishaji, usalama wa mipaka, pamoja na shughuli za kiuchumi na kijamii kwa wakazi wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea.
katika hafla ya kukabidhi rasmi kazi ya ujenzi kwa mkandarasi kutoka kampuni ya China First Highway Engineering Co. Ltd, Mhagama alisema barabara hiyo itarahisisha usafirishaji wa bidhaa kutoka mashambani kwenda masokoni, kuongeza uzalishaji wa mazao ya biashara, pamoja na kuimarisha fursa za uwekezaji kwa wakazi wa maeneo hayo.
"Ni muda wa wananchi kuongeza kasi ya uzalishaji kupitia kilimo, ufugaji na biashara ndogondogo, ili waweze kunufaika na barabara hii ambayo itakuwa mkombozi mkubwa," alisisitiza Mhagama.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Ruvuma, Mhandisi Fedinand Mdoe, aliwahakikishia wananchi 851 waliopisha mradi kuwa watalipwa fidia stahiki kwa wakati bila kuathiri shughuli zao. Alieleza kuwa tathmini ya mali za wananchi hao imeshakamilika na kwamba zaidi ya Shilingi Bilioni 5 zimetengwa kwa ajili hiyo, ambazo zitalipwa mara baada ya TANROADS kupokea fedha kutoka Wizara ya Fedha.
Mhandisi Mdoe alibainisha kuwa mradi huo unatekelezwa kwa ufadhili wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa gharama ya Shilingi Bilioni 110.77, na unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 27. Aidha, aliweka bayana kuwa TANROADS itasimamia kwa karibu utekelezaji wa mradi huo ikiwa ni pamoja na kuweka utaratibu wa kushughulikia malalamiko kupitia kamati maalum.
Halmashauri ya Wilaya ya Songea ni miongoni mwa maeneo yanayotarajia kunufaika kwa kiwango kikubwa kupitia ujenzi huo, hasa kutokana na barabara hiyo kuunganisha vijiji mbalimbali vya vijijini na miji mikubwa ya kibiashara. Mradi huo utafungua lango muhimu la kiuchumi kati ya Wilaya ya Songea na Wilaya ya Nyasa, pamoja na kuwezesha usafirishaji wa watu na bidhaa kati ya Tanzania na Msumbiji kupitia mpaka wa Mkenda.
Akizungumza kwa niaba ya serikali ya wilaya, Mkuu wa Wilaya ya Songea, Kapenjama Ndile, alisema barabara hiyo ni kichocheo muhimu cha maendeleo kwani itahamasisha wawekezaji, kuongeza fursa za ajira, na kurahisisha huduma za kijamii kufika kwa wananchi kwa urahisi. Alisisitiza kuwa ni wajibu wa viongozi na watendaji kuwapa wananchi taarifa za kutosha kuhusu miradi kama hii ili kuimarisha uhusiano kati ya serikali na jamii.
Wananchi wa kijiji cha Litapwasi, miongoni mwa vijiji vinavyonufaika na mradi huo, wameonyesha matumaini makubwa ya kupungua kwa changamoto ya usafiri hasa wakati wa mvua na kiangazi. Bali Tindwa na Felista Luena ni miongoni mwa wakazi waliotoa shukrani kwa serikali kwa kuona hatua ya mradi kuanza rasmi, wakisema kuwa sasa wanaamini ahadi ya maendeleo inatekelezwa kwa vitendo.
Awamu ya kwanza ya mradi huo inajumuisha ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilomita 60 kutoka Likuyufusi hadi Mkayukayu, huku awamu inayofuata ikitarajiwa kuendelea kutoka Mkayukayu hadi Mkenda (km 64), pamoja na ujenzi wa madaraja ya Mitomoni na Mkenda.
Mradi huu mkubwa unatarajiwa kuwa kichocheo kikuu cha maendeleo katika Ukanda wa Kusini, hasa kwa Wilaya ya Songea ambayo sasa inachipua kama kitovu kipya cha biashara, kilimo na usafirishaji mkoani Ruvuma.
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa