SHIRIKA lisilo la kiserikali la TUSOME PAMOJA limetoa mafunzo ya siku moja kwa maafisa habari,maafisa elimu na wenyeviti wa waratibu Elimu kata katika Halmashauri zote nane za mkoa wa Ruvuma,mafunzo hayo yamefanyika kwa siku moja katika Hoteli ya Agapol Matogoro Manispaa ya Songea.
Mafunzo yaliyotolewa kwa maafisa hao yanahusu kuibua na kubadilishana simulizi za mabadiliko chanya katika maeneo yao ambapo wamekubaliana kuweka mpangokazi wa kufanya tafiti katika maeneo yao kwa kuangalia simulizi za mabadiliko chanya,kufanya mahojiano ya wahusika,kukusanya data,kuchambua na kuandika simulizi fupi kwa njia ya machapisho au video kisha kuziwasilisha TUSOME PAMOJA Mkoa wa Ruvuma Oktoba 9 mwaka huu.
Mratibu wa TUSOME PAMOJA katika Mkoa wa Ruvuma Steven Msabaha amesema simulizi za mabadiliko kutoka katika Halmashauri zote za mkoa wa Ruvuma zinatarajiwa kuwasilishwa kimkoa kuanzia Oktoba 16 hadi 17 mwaka huu na kufanyiwa majadiliano ya wanahabari kupitia vyombo vya habari.
Uchunguzi umebaini kuwa simulizi za mabadiliko katika elimu zitasababisha shule nyingine kujifunza kutoka katika shule ambazo zimefanya vizuri na kufanya mabadiliko kwa kuiga au kubadilishana uzoefu wa masuala ya kielimu.
Akitoa historia ya shirika la TUSOME PAMOJA ambalo linafadhiliwa na USAID katika kipindi cha kuanzia Machi 2016 hadi Machi 2021,Mratibu wa TUSOME PAMOJA mkoani Ruvuma,Steven Msabaha amesema shirika hilo kwa sasa linafanyakazi katika mikoa minne ya Tanzania bara ambayo ni Ruvuma,Iringa,Mtwara na Morogoro pia linafanyakazi Tanzania Visiwani.
Msabaha amesema katika Mkoa wa Ruvuma TUSOME PAMOJA inafanyakazi katika Halmashauri zote nane za Mkoa zikiwa na jumla ya kata 173 na shule za msingi 766 na kwamba lengo la shirika hilo ni kushirikiana na serikali kupitia Wizara ya Elimu na TAMISEMI kuhakikisha kuwa katika kipindi cha miaka miwili ijayo wanafunzi wa darasa la kwanza na pili waweze kusoma kwa ufasaha na kwamba hadi sasa TUSOME PAMOJA imetimiza miaka mitatu.
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa