TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoani Ruvuma kwa kipindi cha miezi mitatu imefanya ufuatiliaji wa miradi iliyogharimu kiasi cha fedha Zaidi ya shilingi Bilioni 6.
Hayo yamethibitishwa na Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Ruvuma Janeth Haule wakati akitoa taarifa ya utendaji kazi wa ofisi kwa kipindi cha miezi mitatu kuanzia mwezi Julai hadi Septemba 2022 kwa waandishi wa habari.
Akizungumza katika kikao hicho amesema ufuatiliaji huo umefanyika katika miradi ya ujenzi wa barabara Manispaa ya Songea na Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga kwa thamani ya Bilioni 5,764,392,899.80 na nyumba za Watumishi Wilayani Tunduru na Nyasa zenye thamani ya Shilingi Milioni 125,000,000 pamoja na ujenzi wa shule mpya ya sekondari Wilayani Tunduru wenye thamani ya Shilingi Milioni 470,000,000.
Naibu Mkuu wa TAKUKURU Janeth ameongeza kuwa lengo la ufuatiliaji huo ni kuhakikisha kuwa miradi yote ya Serikali inatekelezwa kwa wakati ikiwa na ubora unaolingana na thamani ya fedha iliyotolewa.
Vilevile amesema TAKUKURU imedhamiria kuendelea kufanya kazi za uzuiaji rushwa kwa lengo la kubaini mianya ya rushwa katika maeneo mbalimbali zikiwemo Taasisi za Umma na Binafsi na kushauri namna bora za kuiziba mianya hiyo.
Hata hivyo ametoa wito kwa Wakurugenzi wa Halmashauri zote za Mkoa wa Ruvuma kuendelea kutoa ushirikiano wa hali ya juu wakati wa kutekeleza miradi ya mpango wa maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya Uviko-19 katika Tawala za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa pindi utakapohitajika.
Janeth amesema kwa mujibu wa kifungu cha 7 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na 11 ya mwaka 2007, TAKUKURU ina majukumu makuu matatu ambayo ni kuelimisha jamii juu ya rushwa na madhara yake, kufanya chambuzi za mifumo kwenye taasisi za umma na sekta binafsi pamoja na kufanya uchunguzi na kufikisha watuhumiwa mahakamani kwa kibali cha Mkurugenzi wa mashtaka baada ya chunguzi hizo kukamilika.
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa