Ikiwa ni zaidi ya miezi miwili tangu kufunguliwa kwa Stendi ya Kisasa ya Mabasi Lundusi, Halmashauri ya Wilaya ya Songea, wananchi wamepata unafuu wa maisha kwani ujio wa Stendi hiyo umerahisha usafir na upatikanaji wa huduma muhimu.
Stendi hiyo imerahisisha usafiri kwa watumishi na wakazi wa Peramiho, Maposeni na Kilagano lakini imewezesha wajasiriamali kuanzisha biashara ndogo ndogo katika maeneo yanayozunguka stendi hiyo.

Wadau mbalimbali wanaonufaika na uwepo wa stendi ya mabasi iliyojengwa katika Kijiji cha Lundusi, Halmashauri ya Wilaya ya Songea, wameeleza kuridhishwa kwao na namna stendi hiyo imeboresha huduma za usafiri na maisha ya kila siku. Wameeleza kuwa stendi hiyo ni ya kisasa na imejengwa kwa kuzingatia mahitaji ya abiria na madereva.
Dereva Bw. Gotadi Mapunda, akizungumza kwa niaba ya wenzake alisema miundombinu na mazingira ya stendi hiyo yamekuwa bora ukilinganisha na maeneo ya awali waliyokuwa wakitumia. Aliongeza kuwa eneo la stendi ni kubwa kiasi cha kuruhusu magari yote kupaki bila usumbufu, jambo linalorahisisha utendaji kazi na kuondoa msongamano.
“Huduma zilizopo ndani ya stendi hii, ikiwemo uwepo wa vyoo, zimechangia kwa kiwango kikubwa kuongeza heshima na ubora wa huduma zetu kwa abiria,” alisema Bw. Mapunda.
Kwa upande wake, Bi. Magreth Nyoni, mmoja wa abiria waliotumia stendi hiyo, alisema uwepo wa stendi hiyo umepunguza gharama na muda waliokuwa wakitumia awali kufuata mabasi mbali na kijiji chao. “Ni faraja kubwa kwetu wananchi wa Lundusi kwani sasa tunapata usafiri karibu na makazi yetu bila usumbufu,” alisema.
Wananchi na wadau wengine wamepongeza uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea kwa kusimamia ujenzi wa stendi hiyo, wakisema imekuwa chachu ya maendeleo na fursa mpya kwa wakazi wa Lundusi na maeneo jirani.
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa