Halmashauri ya Wilaya ya Songea kupitia Idara ya Maendeleo ya Jamii leo Desemba 23, 2025 imetoa mafunzo kwa jumla ya vikundi 83 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu vilivyonufaika na mikopo ya asilimia 10 inayotokana na mapato ya ndani ya Halmashauri.
Mafunzo hayo yamefanyika katika Ukumbi wa Jenista Mhagama uliopo Shule ya Sekondari Maposeni, ambapo jumla ya vikundi 45 vya wanawake, vikundi 30 vya vijana na vikundi 8 vya watu wenye ulemavu vimenufaika na mikopo yenye thamani ya shilingi milioni 726.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea ambaye pia ni Mkuu wa Divisheni ya Maendeleo ya Jamii, Bi. Zawadi Nyoni, amewataka wanufaika hao kudumisha upendo, mshikamano na ushirikiano miongoni mwa wanakikundi ili kuhakikisha miradi wanayoitekeleza inaleta tija na mikopo inarejeshwa kwa wakati.
Bi. Zawadi amesisitiza kuwa fedha zilizotolewa zitumike kwa kuzingatia mchanganuo uliowasilishwa wakati wa kuomba mkopo, pamoja na kuzingatia nidhamu ya matumizi ya fedha. Aidha, amewahimiza wanufaika kurejesha mikopo hiyo kwa wakati ili kuwawezesha wananchi wengine nao kunufaika, akisisitiza kuwa “dawa ya deni ni kulipa.”
Katika mafunzo hayo, elimu mbalimbali zilitolewa kulingana na aina ya miradi inayotarajiwa kutekelezwa na vikundi hivyo. Akitoa elimu ya kilimo, Afisa Kilimo wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea, Ndugu Leonard Mhagama, amewahimiza wanufaika wanaojihusisha na shughuli za kilimo kufanya uchaguzi sahihi wa mashamba, kutumia mbegu bora, kusafirisha pembejeo kwa wakati na kufuata kanuni na taratibu bora za kilimo ili kuongeza uzalishaji na kuhakikisha marejesho ya mikopo yanafanyika kwa wakati.

Kwa upande wa vikundi vya vijana vilivyopanga kutumia mikopo hiyo kununua pikipiki kwa ajili ya biashara ya bodaboda, Afande Ramadhan Duru ametoa elimu ya usalama barabarani, akisisitiza umuhimu wa kuwa na leseni halali ya udereva, kuzingatia sheria za barabarani na kutunza vyombo vya moto ili kudumisha biashara na kuhakikisha marejesho ya mikopo yanaendelea vizuri.
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa