Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Dkt. Louis Chomboko, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, leo Novemba 20, 2025, amepokea jumla ya vitanda 25, magodoro 25 na mashuka 50 kutoka kwa Meneja wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) katika Kituo cha Afya cha Muhukuru Lilahi.
Akizungumza katika hafla ya makabidhiano, Dkt. Chomboko ameishukuru taasisi hiyo kwa kuunga mkono jitihada za Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuiendeleza sekta ya afya, hususani kwa kuleta msaada huo katika kituo hicho kinachohudumia wananchi wa maeneo hayo.
“Binafsi napenda kuwashukuru sana PSSSF kwa kuona umuhimu wa afya za wananchi. Najua vituo ni vingi na mahitaji ni makubwa kila mahali, lakini mmeona ni vyema kuunga mkono kituo hiki ambacho kilikuwa na uhitaji mkubwa, Tunawashukuru sana,” alisema Dkt. Chomboko.

Kwa upande wake, Meneja wa PSSSF Kanda ya Kusini, Bw. Lulyalya Sayi, amesema pamoja na mfuko huo kuwa mpya, umefanikiwa kutoa huduma na misaada kwenye maeneo mbalimbali yenye mahitaji makubwa, na leo umefika Muhukuru Lilahi ili kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha huduma za afya.
“Tunaamini vifaa hivi vitawasaidia wananchi wengi, wakiwemo watumishi wa umma ambao ni wanachama wetu, pamoja na wananchi wengine wa kawaida. Sisi kama mfuko tunaunga mkono jitihada za Mhe. Rais zinazolenga kazi na utu, Wananchi wakitibiwa na kuwa na afya njema, wataweza kufanya kazi ipasavyo,” alisema Bw. Sayi.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea, Bw. Hassan Mtamba, akipokea vifaa hivyo kwa niaba ya Halmashauri, ameishukuru PSSSF kwa kuichagua Songea DC miongoni mwa Halmashauri nyingi za Mkoa huo.
“Tunawashukuru sana kwa msaada huu mkubwa, tunaamini Halmashauri ni nyingi katika Mkoa huu, lakini mmeliona jicho la huruma kufikisha msaada hapa Songea DC. Tunaahidi vifaa hivi tutavitunza na kuvifanya vitumike kwa malengo yaliyokusudiwa ili kuwanufaisha wananchi,”
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa