Kaimu Afisa Mipango wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea, Bi. Prisila Massay, akiambatana na wataalamu wa Halmashauri hiyo, leo Agosti 29, 2025 ametembelea Kata ya Peramiho kwa ajili ya kutambulisha miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa kituo cha afya cha Peramiho na ujenzi wa madarasa pamoja na matundu ya vyoo katika Shule ya Msingi Mnyonga, kijiji cha Nguvumoja.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara, Bi. Massay amewataka wananchi wa kata hiyo kushirikiana kikamilifu katika utekelezaji wa miradi hiyo kwa kuwa itahudumia vijiji vyote vya Peramiho A, Peramiho B, Lundusi na Nguvumoja.

Kwa upande wake, Kaimu Afisa Elimu Msingi, Mwl. Sothery Nchimbi, amesisitiza mshikamano kati ya kamati za ujenzi na wananchi, akisema mchango wa nguvu kazi za wananchi ni nguzo muhimu ya kufanikisha miradi hiyo. Ameeleza pia ni vyema kuwatumia mafundi wazawa ili kuimarisha ubora wa kazi na kuongeza uwajibikaji, lakini kwa sharti la kuwa na vigezo vinavyohitajika kisheria ikiwemo kujisajili kwenye mfumo wa NeST.
Naye Mhandisi Hafidhi Kimaro kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Songea amesema kituo cha afya kitajengwa kwa gharama ya zaidi ya shilingi ya milioni 641 na kitahusisha majengo ya mama na mtoto, maabara ya kisasa, chumba cha upasuaji, jengo la kufulia, jengo la wagonjwa wa nje (OPD) na vyoo.

Aidha, katika Shule ya Msingi Mnyonga, ambayo inahudumia wanafunzi wenye mahitaji maalum, ujenzi utahusisha madarasa mapya mawili, matundu ya vyoo 12 na ukarabati wa shule kwa gharama ya zaidi ya shilingi milioni 131 na ujenzi wa vyoo vingine 21, kwa gharama ya zaidi ya shilingi milioni 49.
Kwa niaba ya wananchi wa Kata ya Peramiho, Mwenyekiti wa Kijiji cha Nguvumoja, Ndugu Lukasi Mselewa, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwaletea miradi hiyo yenye manufaa makubwa kwa wananchi, akisisitiza kuwa itasogeza karibu huduma za afya na elimu kwa wakazi wa eneo hilo.
Miradi hiyo inatarajiwa kukamilika ndani ya miezi mitatu na kuanza kutoa huduma kufikia mwezi Januari mwakani.
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa