Leo Halmashauri ya Wilaya ya Songea inaungana na Watanzania na jamii ya Afrika kwa ujumla kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika, ikiwa ni siku ya kutafakari, kukumbuka na kuchukua hatua juu ya ustawi wa mtoto wa kiafrika.
Katika kuadhimisha siku hii muhimu, Halmashauri ya Wilaya ya Songea inatambua kwa dhati mchango na nafasi ya watoto katika ujenzi wa jamii imara na endelevu. Watoto ni kundi linalopaswa kulindwa, kuelimishwa, na kupewa nafasi ya kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa. Kwa kulitambua hilo, Halmashauri imeendelea kutekeleza mipango mbalimbali inayolenga kuboresha mazingira ya makuzi bora kwa mtoto kijamii, kielimu na kiafya.
Akitoa ufafanuzi Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea Bi Zawadi Nyoni akiwa Ofisi kwake amesema, "Halmashauri imefanikiwa kuimarisha Kamati za Ulinzi wa Mtoto kuanzia ngazi ya vijiji hadi kata, ambazo zimekuwa mstari wa mbele katika utoaji wa elimu ya haki za watoto, uzuiaji wa ukatili, pamoja na kuratibu msaada wa kisheria kwa watoto walioko katika mazingira hatarishi. Aidha, jitihada za kuandikisha watoto wote katika elimu ya awali na msingi zimeendelea kupewa kipaumbele, huku ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya shule ukiimarishwa kila mwaka".
Pia ameeleza kuwa katika sekta ya afya, Halmashauri imehakikisha upatikanaji wa huduma muhimu za afya kwa watoto, ikiwemo chanjo, matibabu ya msingi, na huduma za lishe bora katika vituo vya afya vya serikali. Pia, kupitia programu maalum mashuleni, watoto wamekuwa wakifundishwa stadi za maisha, ujasiri, na umuhimu wa kujitambua mapema ili waweze kuwa viongozi na raia wema wa baadae.
Katika hatua nyingine Bi Zawadi ametoa wito kwa wazazi, walezi, jamii nzima na taasisi zote kuhakikisha kuwa mtoto anapewa haki yake ya msingi haki ya kuishi, kupata elimu, kulindwa dhidi ya ukatili, na kushiriki katika masuala yanayomhusu. "Ulinzi wa mtoto si jukumu la serikali pekee, bali ni wajibu wa kila mmoja wetu katika nafasi aliyonayo".
Tukiwa tunakumbuka historia ya watoto wa Soweto, ni lazima tuiangazie Songea ya leo kwa jicho la matumaini. Mtoto wa Songea ana haki ya kuota ndoto, kujifunza kwa amani, na kukua katika mazingira ya heshima na upendo. Tuendelee kushirikiana kuhakikisha kuwa hakuna mtoto anayebaki nyuma katika safari ya maendeleo.
Kwa pamoja, tuijenge Tanzania mpya kupitia watoto wetu, Siku hii ya mtoto wa Afrika imebeba kauli mbiu isemayo "Haki za Mtoto, Tulipotoka, Tulipo na Tuendako"
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa