Matokeo mazuri ya kidato cha sita mwaka 2025 bado yanaendelea kutazamwa kama kielelezo cha mshikamano mzuri kati ya walimu, wanafunzi, jamii na Serikali kwa ujumla katika Halmashauri ya Wilaya ya Songea.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea Bi Elizabeth Gumbo akitoa vyeti vya pongezi pamoja na fedha taslimu kwa shule tatu za sekondari ambazo zinatoa elimu ya kidato Cha Tano na sita kama motisha na kuwataka walimu hao kuongeza juhudi zaidi katika ufundishaji ili kuleta matokeo bora zaidi kwa mitihani ijayo.

Ili kuunga mkono jitihada hizo, Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kikiongozwa na Mkuu wa Kitengo hicho, Ndugu Augustine Nongwe, kilifanya ziara katika shule tatu za sekondari za Halmashauri ya Wilaya ya Songea zinazofundisha kidato cha tano na sita ambazo ni Mpitimbi, Maposeni, na Jenista Mhagama.
Katika ziara hiyo, Mkuu wa Shule ya Sekondari Mpitimbi, Mwalimu Patrick Matembo, alisema, “Ushirikiano wa karibu kati ya serikali, walimu, jamii na wanafunzi wenyewe ndiyo siri kubwa iliyotuwezesha kupata matokeo mazuri katika mtihani wa kidato cha sita mwaka 2025, Serikali kupitia kutujengea majengo na vifaa bora, pamoja na motisha kutoka kwa Mkurugenzi, imetuwezesha kufanya kazi kwa bidii na kuhakikisha tunapata matokeo chanya.”
Aidha, aliongeza kuwa walimu wa shule hiyo wamekuwa wakijitoa kwa dhati kumaliza mada kwa wakati na kutoa mazoezi ya mara kwa mara, huku jamii ikisaidia kudumisha nidhamu ya wanafunzi.
“Tunalo deni kwa Mkurugenzi wetu na kwa jamii inayotuzunguka, Tunaahidi kuendelea kujipanga vyema na kuhakikisha tunafanya vizuri zaidi katika matokeo yajayo,” alisisitiza Mwalimu Matembo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Sekondari Maposeni, Mwalimu Dismass Nchimbi, naye alisema shule yake imefanikiwa kutokana na nidhamu, mshikamano wa walimu, na juhudi za wanafunzi wenyewe.

“Tumekuwa na utaratibu wa kufuatilia kwa karibu maendeleo ya wanafunzi wetu, kutoa mitihani ya mara kwa mara, kufanya mitihani ya kikanda na kuhakikisha kila mwanafunzi anapata msaada pale anapokwama, hii imekuwa nguzo muhimu ya mafanikio yetu,” alisema
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa