WANANCHI wa vijiji vitatu vya kata ya Liganga na vijiji vingine vinavyopakana na kata hiyo katika Halmashauri ya Wilaya Songea,wanatarajiwa kuondokana na changamoto ya upatikanaji wa huduma ya afya waliyokuwa wanakabiliana nayo kwa muda mrefu, kufuatia ujenzi wa kituo cha afya kinachojengwa katika kata hiyo kukamilika kwa asilimia 98.
Mganga Mkuu wa Halmashauri Dkt Geofrey Kihaule alisema,kituo hicho kinajengwa katika kijiji cha Selekano ambapo kwa gharama ya Sh.milioni 500 ambazo zimetolewa na Serikali kwa awamu mbili.
Dkt Kihaule alisema,katika awamu ya kwanza serikali ilitoa kiasi cha Sh.milioni 250 ambazo zilitumika kujenga jengo la wagonjwa wa nje(OPD)maabara,na kichomoea taka ambapo majengo hayo yamekamilika kwa asilimia 100.
Alisema,majengo hayo yanatarajiwa kufunguliwa katika kipindi cha mwezi mmoja ujao na kuanza kutoa huduma kwa wagonjwa wa magonjwa ya nje wanaofika kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali za matibabu.
Kwa mujibu wa Dkt Kihaule,watumishi watatu watakao fanya kazi katika kituo hicho wameshafika na kwa sasa wapo katika zahanati ndogo ya misheni ya Liganga wakisaidia kutoa huduma kwa wananchi huku wakisubiri kufunguliwa kwa kituo hicho.
Aidha alisema,katika awamu ya pili Halmashauri imepokea jumla ya Sh.milioni 250 kwa ajili ya kujenga majengo pacha ambayo ni ya huduma ya mama na mtoto,upasuaji pamoja na jengo la kufulia ambayo yote kwa sasa yamekamilika.
‘’Naiomba serikali itusaidie kupata vifaa vikiwamo vya maabara mapema ili tuweze kuanza kutoa huduma, kwani majengo yote yamekamilika na kinachosubiri ni kupata vifaa vya upasuaji,maabara na vitanda kwa ajili ya kulaza wagonjwa’’, alieleza Dkt Kihaule.
Alisema,kituo hicho kinatarajiwa kuwahudumia watu wengi zaidi kuliko kituo chochote cha afya katika Halmshauri ya wilaya Songea wakiwamo wafanyakazi zaidi ya elfu nne wa shamba la kahawa la kampuni ya Aviv Ltd ambao wengi wanaishi katika kijiji cha Liganga.
Dkt Kihaule alitaja wanufaika wengine ni wananchi wa kijiji cha Liganga,Selekano,wafungwa na askari wa gereza la Kitai,wafanyakazi wa migodi ya makaa ya mawe,wananchi wa kijiji cha Amanimakoro kilichopo wilaya jirani ya Mbinga, wananchi wa kijiji cha Mbinga Mhalule,Matomondo na Lipokela.
Alisema,kukamilika kwa kituo hicho ni ufumbuzi mkubwa sio kwa wananchi wa kata ya Liganga tu, bali hata kwa watu wengine wanaotumia barabara ya Songea-Mbinga ambao wakipata ajali na shida nyingine watakimbilia katika kituo hicho kwa ajili ya kupata msaada wa matibabu.
Mwenyekiti wa kijiji cha Selekano Magreth Haule,ameishukuru serikali kupitia Halmashauri hiyo kuwajengea kituo cha afya kwani awali walilazimika kutembea umbali mrefu na kutumia gharama kubwa Kwenda kupata matibabu maeneo ya mbali.
Amempongeza Mbunge wa Jimbo la Peramiho na Waziri wa nchi ofisi ya Rais menejimenti ya utumishi wa umma na utawala bora Jenista Joakim Mhagama,kwa kazi nzuri anayofanya ya kuwahudumia wananchi wa jimbo hilo na kutafuta fedha kwaajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.
Pia amewashukuru baraza la Madiwani wakiongozwa na Mhe.Menas Komba, Viongozi wa Chama na Mkurugenzi Ndugu Neema Maghembe kwa usimamizi mzuri wa miradi inayotekelezwa sehemu mbalimbali.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Songea Ndugu Neema Maghembe alisema,tayari wamepokea jumla ya watumishi 39 wa kada mbalimbali katika sekta ya afya ambao wamesharipoti na wanaendelea kufanya kazi ya kuwahudumia wananchi.
Ndugu Neema alisema,katika kipindi cha mwaka mmoja wamepokea Sh.bilioni moja zinazotokana na tozo kwa ajili ya kujenga vituo viwili vya afya katika kata ya Liganga na Mgazini.
Aidha alieleza kuwa, wamepokea fedha nyingine kiasi cha Sh.milioni 500 kwa ajili ya kujenga jengo la upasuaji na majengo mengine katika Hospitali ya Halmashauri iliyopo kijiji cha Mpitimbi ambayo imeshaanza kutoa huduma kwa wananchi wa Songea na wale wanaotoka nchi jirani ya Msumbiji.
Ndugu Neema alisema, katika mkakati wa kusogeza huduma kwa wananchi wamefanikiwa kujenga zahanati katika kijiji cha Ndongosi kwa gharama ya Sh.milioni 50 na zahanati nyingine katika kijiji cha Makwaya kata ya Lilahi ambapo wananchi walilazimika Kwenda maeneo mengine kufuata matibabu.
Pia alisema, wamepokea kiasi Sh.milioni 104 ambazo zitatumika kuboresha mazingira ya kujifungulia kwa akina mama wajawazito katika zahanati mbalimbali ambapo kwa sasa wananchi wa maeneo hayo wanaendelea kufurahia huduma bora za afya.Ndugu Neema amewahasa wananchi kutumia zahanati,vituo vya afya na Hospitali zinazojengwa kwenda kupata huduma bora za afya kwani serikali inatumia fedha nyingi kwa ajili yao na kuachana na mila zilizopitwa na wakati zinazodai.
‘’Nipende kuchukua nafasi hii kuishukuru Serikali ya awamu ya sita ikiongozwa na Mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan pamoja na Mbunge wetu wa Jimbo la Peramiho Jenista Joakim Mhagama kwa kutuletea fedha kwaajili ya kutekelez miradi mbalimbali ya maendeleo’’, amesema Ndugu Neema.
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa