MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas amewataka watumishi kujenga na kuimarisha mahusiano mazuri katika sehemu za kazi na kufanya kazi kwa kushirikiana baina ya wakuu wa Idara na Watumishi wa chini.
Ameyasema hayo wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea katika ukumbi wa mikutano wa Lundusi-peramiho.
RC Thomas amewasisitiza watumishi wa umma kutokua sehemu ya kuhujumu miradi ya maendeleo kwani serikali haitasita kuchukua hatua kwa mtumishi yoyote ambaye anakwenda kinyume na sharia za Utumishi wa umma.
‘’Nawasisitiza muwe wasimamizi wazuri wa miradi ili iweze kukamilika kwa wakati na viwango vinavyokubalika na serikali, hii inaleta motisha hata kwa serikali yetu kuendelea kuleta fedha kwaajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo’’, amesisitiza RC Tomas.
Aidha amewashauri watumishi kujiepusha na mikopo yenye riba kubwa pia wapunguze kuishi maisha feki kwani yanasababisha kuingia kwenye madeni makubwa ambayo ni hatari kwa mtumishi.
Vilevile ameuagiza uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea kuanzisha mashamba ya pamoja (Block farming) na kusisitiza kuwa Serikali inaendelea kuboresha mfumo wa usambazaji mbolea ya ruzuku ili kusogeza jirani na wakulima.
Pia RC Thomas amepiga marufuku uingizaji wa mifugo katika maeneo ya vijiji kwani inaweza leta migogoro kati ya wakulima na wafugaji hivyo amewataka viongozi wa kata na kijiji kuendelea kufanya jitihada za kuondoa mifugo hiyo.
Hata hivyo Mkuu wa Mkoa ameupongeza uongozi wa Halmashauri kwa ubunifu wa vyanzo vipya vya kuingiza mapato na kwa usimamizi mzuri wa miradi ya serikali hii itasaidia Halmashauri kwenda mbele Zaidi.
Akizungumza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea Ndugu Neema Maghembe ameahidi kutekeleza maagizo yote yaliyotelewa na Mkuu wa Mkoa.
Amesema ukusanyaji wa mapato katika Halmashauri unaridhisha ambapo kwa mwaka wa fedha 2021/2022 Halmashauri ilikusanyia shilingi bilioni 1.7 sawa na asilimia 115.
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa