MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas amezindua zoezi la upandaji miti kimkoa katika chanzo cha mto Mgugusi kinachopatikana katika hifadhi ya Lugumbilo Kijiji cha Mbinga Mharule.
Uzinduzi huo umefanyika leo kwa kupanda Miche ya miti 2000 na kuudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Mkoa wa Ruvuma na wa Wilaya ya Songea.
Akizungumza katika uzinduzi huo amewataka wananchi wote wanaojishughulisha na kilimo katika eneo hilo la hifadhi waondoke mara moja.
Aidha, amewataka wananchi waendelee kutunza mazingira,vyanzo vya maji vyote pamoja na misitu kwani inafaida kubwa sana katika maisha ya binadamu.
“ Nawaomba kila mtu kwa nafasi yake hata kama ni nyumbani kwake pandeni miti isimamieni ili kuhakikisha miti inaota na sisi kama Viongozi tutapita kuangalia na kwa wale watakaofanya vizuri tutatoa zawadi” , amesisitiza RC Thomas.
RC Thomas ametoa rai kwa wananchi na Viongozi kuhakikisha katika vituo vya Afya na Taasisi zote za Serikali kuwe na utaratibu wa kupanda miti wakati majengo yanajengwa Ili yakikamilika yawe yamezungukwa na mandhari nzuri.
Kwaupande wake Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Ruvuma Ndugu Odo Mwisho amesema Ilani ya Chama ya mwaka 2020-2025 inahimiziza utunzaji wa mazingira na hifadhi za vyanzo vya maji hivyo wananchi waendelee kupanda miti kwenye maeneo yasiyo na miti na hata yenye miti.
“ Nawasihi Viongozi wenzangu tupite katika maeneo yote ambayo ni hifadhi za maji tukatoe angalizo kwa wananchi wasilime katika maeneo hayo ili tuendelee kutunza vyanzo vyetu vya maji”, amesema Ndugu Mwisho.
Nae Mkuu wa Wilaya ya Songea Mheshimiwa Pololet Kamando Mgema amesema hatua ya Kwanza itakayochukuliwa ni kufufua mipaka ya hifadhi ili wananchi wasiseme hawajui hifadhi inaishia wapi kwa kushirikiana na wakala wa misitu TFS pamoja na watu wa bonde ili wananchi wananchi waliopo katika eneo la hifadhi waondoke.
“Kila hifadhi imepakana na Kijiji na kila Kijiji kuna Viongozi na kamati za utunzaji wa mazingira hivyo mnawajibu wa moja kwa moja wa kuhakikisha kwamba wananchi wanatunza maeneo ambayo yalitengwa na yakachaguliwa kwaajili ya kuwa hifadhi”, amesema Mhe. Mgema.
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa