Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Ahmed Abasi Ahmed, leo Januari 6, 2026, amefanya ziara ya kikazi katika Halmashauri ya Wilaya ya Songea, ambapo amekagua utekelezaji wa miradi mitatu ya maendeleo katika sekta ya elimu inayotekelezwa katika Halmashauri hiyo.
Ziara hiyo imelenga kutathmini maendeleo ya miradi, ubora wa ujenzi pamoja na matumizi ya fedha za Serikali na wadau wa maendeleo.
Katika ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa alianza ukaguzi wake katika Shule ya Sekondari Jenista Mhagama, ambako alikagua ujenzi wa mabweni mawili, madarasa sita pamoja na matundu kumi ya vyoo. Ujenzi wa miundombinu hiyo unagharimu jumla ya shilingi milioni 417 za Kitanzania, kwa ufadhili wa BARRIC ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali katika kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.

Aidha, ukaguzi uliendelea katika Shule ya Sekondari Amali Lundusi, ambapo Mkuu wa Mkoa alikagua ujenzi wa miundombinu mbalimbali ikiwemo jengo la utawala, vyoo vya wavulana na wasichana matundu 6, madarasa nane, nyumba ya mwalimu, maktaba pamoja na jengo la TEHAMA. Miradi hiyo kwa pamoja inagharimu jumla ya shilingi milioni mia tano na hamsini, huku shule hiyo ikiwa katika hatua ya mwisho ya ukamilishaji wa ujenzi.
Ziara hiyo ilihitimishwa katika Shule ya Msingi Mnyonga, ambako alikagua ukarabati wa madarasa yaliyopo, ujenzi wa madarasa mapya pamoja na ujenzi wa matundu ya vyoo. Miradi hiyo, inagharimu takribani shilingi milioni 132 kwa ufadhili wa programu za BOOST pamoja na SWASH.
Akizungumza wakati wa ukaguzi huo, Brigedia Jenerali Ahmed Abasi Ahmed alisema kuwa Serikali inaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo yenye matokeo chanya yanayoonekana moja kwa moja kwa wananchi, huku matokeo yake yakionekana wazi katika Mkoa wa Ruvuma, hususan katika sekta ya elimu. Hivyo aliwataka wasimamizi wa miradi hiyo kuharakisha miradi hiyo ili iweze kutumika kwa mapema iwezekanavyo
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea, Mheshimiwa George Ponera, kwa niaba ya wataalamu wa Halmashauri hiyo, alipokea maelekezo yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa na kuahidi kuyatekeleza kwa ufanisi.
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa