Kamati ya maandalizi ya Tamasha la Tatu la Utamaduni na maandalizi ya uchaguzi wa serikali za mitaa, ikiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Mhe. Ahmed Abbas Ahmed, imefanya kikao muhimu katika ukumbi wa Manispaa ya Songea ili kujadili mikakati ya kufanikisha matukio hayo mawili makubwa.
Mhe. Ahmed alifungua kikao kwa kufikisha salamu za Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, akieleza kuwa, "Rais wetu anafanya kazi bila kupumzika kuhakikisha miradi ya maendeleo ya wananchi inapata fedha za kutosha. Anatutaka tuhakikishe fedha hizo zinatumika vyema kukamilisha miradi kwa ajili ya ustawi wa wananchi."
Akizungumzia maandalizi ya Tamasha la Utamaduni, Mhe. Ahmed alieleza kuwa maandalizi yamefikia hatua nzuri na kuwaomba wote kushirikiana kama timu moja ili kufanikisha tukio hilo. Aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi na kuomba kwa Mungu ili tamasha liende salama na kwa amani.
Katika maandalizi ya uchaguzi wa serikali za mitaa, Mkuu wa Mkoa alisisitiza umuhimu wa kuwahamasisha wananchi kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura na kushiriki kikamilifu katika uchaguzi utakaofanyika tarehe 27 Novemba. Aidha, aliwahimiza watu wenye sifa kujitokeza kugombea nafasi za uongozi ili kuhakikisha tunapata viongozi wenye uwezo wa kuleta maendeleo ya kweli.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Songea, Mhe. Wilman Kapenjama Ndile, aliwakaribisha wananchi kutoka ndani na nje ya nchi kushiriki katika Tamasha hilo la kihistoria. Alisema kuwa maandalizi ya tukio hilo yanazingatia usalama na kwamba wageni watapata huduma bora za malazi na usalama. "Nawaomba mjitokeze kwa wingi kuanzia siku ya ufunguzi hadi siku ya kilele cha Tamasha ," alisema.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma, Bi. Mary Makondo, aliwasilisha taarifa ya maandalizi, akieleza kuwa kutakuwa na siku nane za maandalizi, zikiambatana na midahalo ya wanafunzi, mashindano ya ngoma za asili, maonyesho ya magari ya zamani, mdahalo wa kiutamaduni, na mashindano ya mpira wa miguu.
Wadau mbalimbali waliohudhuria kikao hicho walipongeza juhudi za kuandaa Tamasha hilo, wakisema kuwa litatoa fursa nyingi za kiuchumi na kimaendeleo. Waliomba juhudi zaidi zifanywe kuhamasisha uchangiaji wa michango kutoka kwa wadau, hususani wawekezaji, ili kufanikisha tukio hilo kwa kiwango cha juu zaidi na kuiweka Ruvuma katika ramani ya matukio makubwa ya utamaduni nchini.
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa