Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea Bi Elizabeth Gumbo amegawa vishikwambi kwa Maafisa Ugani Kilimo wa Halmashauri hiyo kama sehemu ya mkakati wa serikali wa kuboresha sekta ya kilimo nchini Tanzania.
Akiwa kwenye hafla ya kukabidhi vifaa hivyo, Bi Gumbo alisema kuwa serikali imekuwa mstari wa mbele kuwekeza katika sekta ya kilimo kwa kutoa vifaa muhimu kama pikipiki, raincoat, viatu, na vifaa vya kupima udongo, ambavyo vitasaidia maafisa kilimo kufanya kazi kwa ufanisi zaidi. "Hii ni sehemu ya dhamira ya serikali kuhakikisha maafisa kilimo wanawafikia wakulima kwa urahisi, wakitoa ushauri wa kitaalamu na kusaidia kuimarisha uzalishaji wa mazao," alieleza.
Mkurugenzi huyo aliongeza kuwa lengo la serikali ni kuwasaidia wananchi kuboresha kipato kupitia kilimo na kuwawezesha kuondokana na umasikini. Alisema kuwa vishikwambi hivi vimesajiliwa rasmi na vimeunganishwa na mifumo ya taarifa za kitaifa ili kuwezesha ufuatiliaji wa taarifa za wakulima katika ngazi zote. "Vishikwambi hivi vitawawezesha maafisa kilimo kusajili wakulima, kutuma taarifa zao kwa urahisi, na kusaidia kufuatilia maendeleo ya shughuli za kilimo hadi makao makuu."
Aidha, aliwahimiza maafisa Ugani kilimo kutumia vifaa hivyo kwa uadilifu na kuacha tabia ya kuvifungia ndani. Alisisitiza kuwa vifaa hivyo ni mali ya umma na vinapaswa kutumika kwa manufaa ya wananchi. “Tusije tukafunga vifaa hivi ndani na kuendelea na shughuli zetu binafsi. Maafisa kilimo wana wajibu wa kwenda kwa wananchi na kuhakikisha vifaa hivi vinatumika kuongeza tija katika sekta ya kilimo ambayo ni tegemeo kubwa kwa Halmashauri yetu,” aliongeza.
Kwa hatua hii ya kugawa vishikwambi na vifaa vingine muhimu, serikali imeonesha dhamira ya dhati ya kuinua hali za wananchi kupitia sekta ya kilimo. Serikali imedhamiria kuhakikisha kuwa wataalamu wa kilimo wanapata rasilimali wanazohitaji ili kuwasaidia wakulima kuongeza uzalishaji, kuongeza kipato na hatimaye kuboresha maisha yao.
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa