Agosti 24, Kaimu Afisa Elimu Msingi wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea, Ndugu Solteri Nchimbi, kwa kushirikiana na wataalamu kutoka Halmashauri hiyo, wametambulisha rasmi mradi wa ujenzi wa shule mpya ya awali na msingi katika kijiji cha Magagula, Shule hiyo itakayojengwa katika eneo la shule ya sekondari Magagula inatarajiwa kugharimu jumla ya shilingi milioni 311.
Akihutubia wananchi katika mkutano wa hadhara, Nchimbi alisema kuwa ujenzi wa shule hiyo ni sehemu ya mikakati ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kukuza elimu kwa watoto wa Tanzania. Alisisitiza ushirikiano wa wananchi katika utekelezaji wa mradi huo, akieleza kuwa shule hiyo inatarajiwa kukamilika na kuanza kutumika ifikapo Januari 2026.
Kwa upande wake, Kaimu Afisa Mipango wa Halmashauri hiyo, Bi Sylvia Festo, aliwahimiza wananchi kushirikiana kwa karibu na kamati ya ujenzi pamoja na wataalamu wa Halmashauri. Alisema wananchi wanapaswa kufuatilia maendeleo ya mradi huo na kutoa taarifa pindi changamoto zitakapojitokeza ili kupatiwa ufumbuzi mapema.

Naye Afisa Manunuzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea, Ndug Raymond Aloyce, alisisitiza kamati ya ujenzi kuzingatia sheria na taratibu za manunuzi kupitia mfumo wa kidijitali wa NeST, ambao unaweka wazi mchakato mzima wa manunuzi. Aidha, alibainisha kuwa hata mafundi wanaotarajiwa kushiriki katika ujenzi huo watapaswa kuomba kupitia mfumo huo kwa kuzingatia vigezo husika.
Kwa upande mwingine, Mhandisi Hafidhi Kimaro kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Songea alikumbusha wajibu wa kuzingatia BOQ (Bill of Quantities) zilizopangwa, ili kuhakikisha ujenzi unakuwa wa kiwango bora na wenye tija kwa vizazi vinavyotarajiwa kunufaika na shule hiyo.
Pia katika mkutano huo wananchi waliweza kuunda kamati ya ujenzi wa Mradi huo ili kufanikisha mradi. Mradi huo unatarajia kujumuisha ujenzi wa miundombinu muhimu ikiwemo madarasa, ofisi pamoja na vyoo, hatua itakayosaidia kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa watoto wa kijiji cha Magagula na maeneo jirani.
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa