KATIBU wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Ruvuma Ndugu Pazza Mwamlima amewataka Wataalamu wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa na kuzingatia uchumi wa mwananchi mmoja mmoja.
Ameyasema hayo leo wakati akizungumza na viongozi na wataalamu wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea katika ukumbi wa mikutano Ofisi ya Mkurugenzi.
‘’Tunatarajia matokeo mazuri katika kila sekta hivyo nawasihi muendelee kufanya kazi vizuri na kwa bidii huku mkishirikiana hakika mtasonga mbele kwa maendeleo’’, amesema Ndugu Mwamlima.
Pia amesema uchumi wa nchi unategemea sana ardhi hivyo amewataka Maafisa wa kilimo kushirikiana vizuri na wananchi katika maswala ya pembejeo maana wakilisimamia hilo vizuri Halmashauri itafika mbali.
Kwaupande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea Mheshimiwa Menace Komba amemshukuru Katibu wa CCM Mkoa kwa kuja kuitembelea Halmashauri Ya Wilaya ya Songea
‘’Ndugu Katibu nakushukuru sana umetutia nguvu, kama rasilimali tunazo tumepokea maelekezo tunakuahidi tutatekeleza hatutakuangusha ‘’, amesema Mheshimiwa Menace.
Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea Ndugu Neema Maghembe ameishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan na Mbunge wa Jimbo la Peramiho Mheshimiwa Jenista Mhagama kwa kuikumbuka Halmashauri kwa kutekeleza Miradi mbalimbali.
‘’Nawaomba timu ya Menejimenti ya wataalamu kufanya kazi kwa weredi na kusimamia utekelezaji wa Miradi yote ambayo inatekelezwa katika Halmashauri yetu tuweze kufika mbali’’, amesisitiza Ndugu Neema.
Imeandaliwa na Bahati Nyoni,
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini.
Septemba 06, 2022.
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa