KAMPUNI ya Songea Sukari Limited ambayo ni moja ya Kampuni tanzu ya Madhvan Group Limited iliyopo nchini Uganda wamefanya mazungumzo na Viongozi kutoka Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Viongozi kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Songea, Viongozi wa Kata na Kijiji pamoja na watumishi.
Lengo la mazungumzo hayo ni kuwasilisha maombi ya ardhi hekta 44,000 katika Kijiji cha Magwamila ambayo itatumika kwaajili ya uwekezaji wa kilimo cha miwa na uwekezaji wa kiwanda cha sukari.
Akizungumza Kapil Dave amesema katika uwekezaji huo wataanza na hekta 3500 ambapo wao watalima miwa kidogo hivyo wananchi watapewa fursa ya kuzalisha miwa mingi zaidi.
Ameongeza kuwa uwekezaji huo utatoa fursa za ajira kwa watu 5000 watakaofanya kazi za kilimo na kiwandani, pia watatoa fursa za ajira za madereva kwa magari 300 ambayo yatatumika kusafirisha zao hilo la miwa.
Aidha, amesema kutokana na uwekezaji wa kiwanda cha miwa watazalisha viwanda vingine vinavyotokana na zao la miwa kama kiwanda cha utengenezaji wa mbolea, pombe kali, pipi pamoja na uzalishaji wa umeme na gesi.
Amesema katika uwekazaji huo watajenga shule za msingi na sekondari pamoja na hospitali ili wananchi ambao watakua wanafanya kazi katika mashamba hayo waweze kupata huduma za kijamii katika maeneo hayo.
Akizungumza Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri Mheshimiwa Simon Kapinga ambaye amemwakilisha Mwenyekiti amesema kwa kushirikiana na Viongozi wa Kata na Kijiji atahakikisha wanapita katika kijiji chote kuongea na wananchi juu ya suala hilo ili waweze kutoa maamuzi ya maombi hayo.
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa