KAMATI ya Siasa Wilaya ya Songea chini ya Mwenyekiti wake Mhe. Thomas Masolwa imetembelea miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Songea kwa lengo la kujiridhisha na hatua za utekelezaji, viwango vya ubora pamoja na thamani ya fedha.
Akiwa katika ziara hiyo, Mhe. Masolwa amesema usimamizi na ufuatiliaji wa miradi ni muhimu sana hasa ikizingatiwa lengo la Serikali ni kuhakikisha inafikisha huduma kwa wananchi wake hivyo miradi isimamiwe ili iweze kukamilika mapema.
"Sisi kama Kamati ya siasa ya Wilaya, jukumu letu ni kuhakikisha miradi inatekelezwa kama maelekezo ya Serikali yanavyotolewa hivyo mafundi Viongozi hakikisheni miradi inakamilika kwa haraka na viwango vinavyokubaliwa na Serikali” amesisitiza Mhe. Masolwa.
Miradi iliyotembelewa ni pamoja na ujenzi wa madarasa 12 katika shule ya Sekondari Jenista Mhagama, mabweni 4 na vyoo matundu 20 unaogharimu fedha kiasi cha shilingi milioni 834 kutoka Serikali Kuu, ujenzi wa shule ya msingi mpya ya Nambalapi inayogharimu fedha kiasi cha shilingi milioni 331.1 kutoka Serikali kuu kupitia mradi wa BOOST na mwisho walitembelea shule ya Sekondari Maposeni ambapo kuna ujenzi wa madarasa 4, mabweni 2 na vyoo matundu 6 unaogharimu fedha kiasi cha shilingi milioni 362.2 kutoka katika kampuni ya Barrick Gold Mine.
Aidha, Mhe. Masolwa ameipongeza na kuishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Mbunge wa Jimbo la Peramiho Mhe. Jenista Joakim Mhagama kwa kuendelea kuleta fedha za kuboresha miundombinu ya Elimu.
Vilevile Mheshimiwa Masolwa amewapongea Baraza la Madiwani, timu ya wataalamu ngazi ya Halmashauri, Kata na Vijiji pamoja na viongozi wote kwa usimamizi mzuri wa miradi.
Kwaupande wake Mwenyekiti wa Halmashauri Mheshimiwa Menas Komba amesema Halmashauri imejipanga vizuri katika kuisimamia miradi ili ikamilike kwa viwango vinavyokubaliwa ili Serikali iendelee kuleta fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi mingine ya Maendeleo.
Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea Ndugu Neema Maghembe ametoa rai kwa mafundi Viongozi kufanya kazi na waache tamaa ya kupokea miradi zaidi ya mmoja ili kuepuka kuchelewa kukamilika kwa miradi.
Ziara hiyo imehusisha Kamati ya siasa ya Wilaya, Mwenyekiti wa Halmashauri, Mkurugenzi Mtendaji na Wakuu wa Idara na Vitengo.
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa