Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango (KFUM) ya Halmashauri ya Wilaya ya Songea, ikiongozwa na Mwenyekiti wake ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri, Mhe. Menans Komba, imefanya ziara ya ukaguzi wa miradi mitano ya maendeleo leo, tarehe 3 Septemba 2024. Ziara hii ililenga kukagua utekelezaji na maendeleo ya miradi hiyo katika maeneo mbalimbali ndani ya halmashauri ya wilaya hiyo.
Kamati ilianza ziara yake kwa kukagua ghala la mazao lililopo katika Kata ya Mbinga Mhalule, Kijiji cha Matomondo. Ghala hili ni muhimu kwa ajili ya kuhifadhi mazao ya wakulima wa eneo hilo, lakini ujenzi wake umekwama kutokana na uhaba wa fedha. Kamati ilijadili makadirio ya fedha zinazohitajika kukamilisha ujenzi huo, ambapo Mwenyekiti alisisitiza umuhimu wa kuhakikisha rasilimali zinapatikana ili kukamilisha mradi huo haraka.
Kamati iliendelea na ziara kwa kukagua ujenzi wa matundu nane ya vyoo kwa wasichana katika Shule ya Msingi Matomondo. Mradi huo ulipokea shilingi milioni 14 kutoka Serikali Kuu. Hata hivyo, ujenzi umesimama ukisubiri kufunguliwa kwa bakaa. Pamoja na changamoto hizo, mradi uko katika hatua za mwisho za kukamilika.
Katika Kijiji cha Kizuka, kamati ilikagua mradi wa uboreshaji wa zahanati ya kijiji hicho, ambao ulipokea fedha katika mwaka wa fedha 2021/2022. Uboreshaji huo unalenga kuboresha chumba cha mama na mtoto, choo na bafu, pamoja na ujenzi wa matundu saba ya vyoo. Mradi huo umegharimu kiasi cha shilingi milioni 27.4, lakini bado haujakamilika. Mwenyekiti wa kamati, Mhe. Komba, alipendekeza tathmini ya gharama zinazohitajika ili kukamilisha ujenzi huo na tathimini ya gharama hizo ziwasilishwe siku ya majumuisho ili fedha zitolewe kukamilisha mradi huo.
Ziara hiyo pia ilijumuisha ukaguzi wa ujenzi wa matundu 13 ya vyoo, kitakasa mikono, pamoja na mnara wa tenki la maji katika Shule ya Msingi Jenista. Aidha, kamati ilikagua Zahanati ya Mipeta ambapo miradi hiyo yote ipo katika hatua za ukamilishaji.
Mwenyekiti wa Kamati, Mhe. Menans Komba, amewataka watumishi wanaosimamia miradi hii kuwa waaminifu na wenye uadilifu katika usimamizi wa miradi ya serikali. Aliongeza kuwa ucheleweshaji wa kukamilika kwa miradi hiyo unachelewesha maendeleo kwa jamii, hivyo ni muhimu kuharakisha utekelezaji wake ili kuboresha maisha ya wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea.
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa