Katika kuelekea msimu mpya wa kilimo, Halmashauri ya Wilaya ya Songea kupitia Idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi imeendelea na zoezi la upimaji wa afya ya udongo ili kuhakikisha wakulima wanapata mbinu sahihi za uzalishaji zitakazoongeza tija na faida katika kilimo chao.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Afisa Kilimo wa Halmashauri hiyo, Ndugu Godson Msalilwa, alisema Serikali imejipanga kuwasaidia wakulima kulima kisayansi na kwa ufanisi kupitia huduma za upimaji wa udongo.
“Kwa kupima afya ya udongo, mkulima atajua aina ipi ya mbolea inahitajika na kwa kiwango gani kulingana na mahitaji ya shamba lake. Hii itasaidia kuepusha upotevu wa rasilimali na kuongeza mavuno,” alisema Msalilwa.

Aidha, ametoa wito kwa wakulima wote wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea kuwatembelea maafisa kilimo wa kata zao ili kuchukua sampuli za udongo kwenye mashamba yao na kuziwasilisha katika Ofisi ya Kilimo ya Halmashauri kwa ajili ya kupimwa. Alibainisha kuwa zoezi hilo ni bure na wakulima hawatozwi gharama yoyote.
Katika hatua nyingine, Msalilwa aliishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Kilimo kwa kuwapatia kifaa maalum cha kisasa cha kupima udongo (Soil Scanner), akieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kuongeza uzalishaji, kuimarisha kilimo cha kisasa na kuchochea maendeleo ya wakulima katika Wilaya ya Songea.
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa