Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma, Bi Marry Makondo, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas Ahmed, ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Songea kwa kupata hati safi katika ukaguzi wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2023/2024.
Bi Makondo alitoa pongezi hizo leo Juni 18, 2025 wakati wa Mkutano maalum wa Baraza la Madiwani uliofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ambapo alisoma hotuba kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa. Alimpongeza Mwenyekiti wa Halmashauri, madiwani wote, pamoja na kumtambua Mbunge wa Jimbo la Peramiho kwa mchango wake katika kufanikisha hati hiyo safi.
"Hati hii safi imepatikana kutokana na juhudi zenu za pamoja katika kujibu na kutetea hoja za Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali," alisema Bi Makondo.
Katika mkutano huo, ilielezwa kuwa kati ya hoja 32 zilizotolewa na Mkaguzi Mkuu, hoja 18 tayari zimefungwa, hoja 14 zipo katika hatua za utekelezaji, na hoja 7 kutoka miaka ya nyuma bado hazijatekelezwa kikamilifu.
Katika hatua nyingine, Bi Makondo aliwapongeza wataalamu wa Halmashauri kwa uwajibikaji mzuri na kuwapatia vyeti vya pongezi watumishi waliofanya vizuri. Watumishi waliotunukiwa vyeti ni Hadija Boffu (Mweka Hazina), Ignus Kong’oa (Mkaguzi wa Ndani), Nurdin Seleman na Lameck Joshua (Wahasibu). Alisema kuwa vyeti hivyo vitachochea ari ya utendaji bora kazini.
Akiwasilisha taarifa ya hoja za CAG kwa mwaka 2023/2024, Mkaguzi wa Ndani wa Halmashauri, Bw. Ignus Kongowa, alieleza kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Songea imeendelea kufanya vizuri ambapo imepata hati safi kwa miaka mitatu mfululizo: 2021/2022, 2022/2023, na sasa 2023/2024, jambo linaloonyesha juhudi kubwa katika kujibu hoja za ukaguzi.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea, Mhe. Simon Kapinga, akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Halmashauri, alitoa shukrani kwa kamati zote za madiwani kwa juhudi zao zilizowezesha Halmashauri kupata hati hiyo safi. Aidha, alimhakikishia Mkaguzi wa Nje kuwa hoja zilizobaki zitafanyiwa kazi ipasavyo ili Halmashauri iendelee kupata hati safi kwa miaka ijayo.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea, kwa niaba ya timu nzima ya watendaji, aliwashukuru wote waliochangia mafanikio hayo. Aliahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Mkaguzi wa Nje katika kuhakikisha hoja zote zinazobakia zinafutwa, sambamba na kuwashukuru Waheshimiwa Madiwani kwa ushirikiano mkubwa waliompatia katika kipindi chao cha uongozi.
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa