Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea, Bi Elizabeth Mathias Gumbo, amewapongeza Wataalamu wa Idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa kufanya vyema na kushika nafasi ya pili, kati ya halmashauri nane zilizopo mkoa wa Ruvuma, katika Maonesho ya Nanenane ambayo Kimkoa yalifanyika Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga.
Akizungumza mara baada ya kupokea cheti hicho, Bi Elizabeth aliwashukuru watumishi wa idara ya kilimo, mifugo na uvuvi kwa kuiwakilisha vyema Halmashauri, akibainisha kuwa mafanikio hayo yametokana na mshikamano wa timu nzima kutoka Idara ya hiyo.

“Natumia fursa hii kuwapongeza idara ya kilimo kwa kufanya vizuri katika maonesho haya, Hii inaonesha mshikamano mlionao ndio umesababisha kufanya vizuri katika maonesho haya. Niwaombe taaluma mliyoionesha kwenye maonesho hayo muihamishie kwa wakulima wetu ili kuongeza tija katika kilimo, hususani tunapoelekea msimu mpya wa kilimo,” alisema Bi Elizabeth Gumbo
Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Ndugu Godson Msalilwa, alisema siri ya ushindi huo ni mshikamano na ushirikiano wa karibu baina ya wataalamu wote wa idara hiyo.
Alifafanua kuwa maonesho hayo, yaliyofanyika katika Viwanja vya Amani Makolo, Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga, yalitoa nafasi kwa Halmashauri ya Songea kuonesha teknolojia mbalimbali ikiwemo uzalishaji wa mazao ya bustani, ufugaji wa sungura na kuku, pamoja na usindikaji wa mazao ya mihogo kwa vikundi vya usindikaji.
Maonesho ya Nanenane hufanyika kila mwaka kwa lengo la kutoa elimu, kuonesha ubunifu na kuhamasisha maendeleo ya sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi nchini ambapo maonesho ya mwaka huu 2025 yamebeba kauli mbiu isemayo "Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo Mifugo na Uvuvi 2025”
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa