Idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ya Halmashauri ya Wilaya ya Songea imeendesha zoezi la ugawaji wa mbegu za mahindi lishe na maharagwe lishe kwa kaya maskini, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhamasisha ulaji wa lishe bora kwa jamii.
Zoezi hilo limefanyika katika vijiji vya Maposeni na Morogoro, ambapo wananchi walipatiwa mbegu hizo kwa lengo la kuwawezesha kuzalisha mazao yenye virutubishi muhimu kwa ajili ya kuboresha afya za familia zao.
Akizungumza wakati wa ugawaji wa mbegu hizo, Afisa Kilimo wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea, BI. Faraja Kiula, alisema kuwa ulaji wa lishe bora unaozingatia makundi ya chakula ni msingi muhimu wa kuimarisha afya ya mwanadamu.
Alieleza kuwa kaya zinapaswa kuzingatia mchanganyiko sahihi wa vyakula ili kupata virutubishi vyote muhimu vinavyosaidia kuimarisha kinga ya mwili na kuzuia magonjwa yanayotokana na upungufu wa lishe.
Bi. Faraja Kiula alibainisha kuwa mbegu za mahindi na maharagwe zilizogawiwa zimeongezewa virutubishi vya zinc na iron kwa kiwango kikubwa, ambavyo ni muhimu kwa afya ya binadamu, hususan kwa watoto na wanawake wajawazito.
Kwa mujibu wake, matumizi ya mbegu hizo yatachangia kupunguza changamoto ya upungufu wa damu na kuongeza nguvu na ustawi wa mwili kwa wananchi watakaonufaika.
Wananchi wa vijiji vilivyonufaika wamepongeza jitihada za Halmashauri, wakisema kuwa zoezi hilo litawasaidia kuboresha uzalishaji wa mazao ya lishe na kuinua hali ya afya na maisha yao kwa ujumla.
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa