Halmashauri ya Wilaya ya Songea kupitia Idara ya Afya, leo Septemba 29, 2025 imeendesha mafunzo ya uongezaji virutubisho kwenye chakula kwa ajili ya kuboresha lishe na afya za wananchi.
Mafunzo hayo yalifunguliwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Dkt. Scholastica Mapunda.
Akizungumza katika ufunguzi huo, Dkt. Mapunda alisisitiza umuhimu wa matumizi ya virutubishi kupitia mashine za kusaga nafaka, akieleza kuwa serikali kwa kushirikiana na Wizara ya Afya imejipanga kuhakikisha lishe bora inapatikana kwa wananchi wote ili kupunguza tatizo la udumavu na maradhi yanayotokana na lishe duni.

Aidha, alitoa wito kwa watendaji kusimamia sheria na kanuni zitakazohakikisha mashine mpya za kusaga nafaka zinazoongeza virutubishi zinafanya kazi ipasavyo, ili unga utakaopatikana uwe na viwango vya afya vinavyohitajika.
Kwa upande wake, Afisa Lishe wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea, Bi. Joyce Sipira, aliainisha aina za virutubishi vinavyoongezwa kwenye chakula ikiwemo zinki, folic acid, madini chuma na vitamin B12. Alieleza kuwa upungufu wa virutubisho hivyo unaweza kusababisha matatizo ya kiafya kama vile mgongo wazi, kichwa kikubwa na mdomo sungura kwa watoto, pamoja na utapiamlo kwa watu wazima.

Bi. Sipira pia aliwataka watendaji kuwa mabalozi wa elimu hiyo kwa wananchi, kwa kuondoa dhana potofu zinazohusiana na matumizi ya virutubishi.
Washiriki wa mafunzo hayo nao walipata nafasi ya kutoa shukrani, ambapo kwa niaba ya wasindikaji wa nafaka, Bw. Betodi Joseph alisema, “Tunashukuru sana kwa mafunzo haya, kwani kupitia mitambo hii mipya tunatarajia jamii yetu itapata unga wenye ubora na hivyo kuwa na afya bora.”
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa