Halmashauri ya Wilaya ya Songea imeadhimisha Siku ya Lishe Kitaifa katika Kata ya Mpitimbi, ikitoa wito kwa wananchi kuzingatia lishe bora kama msingi wa afya na maendeleo ya jamii.
Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri hiyo, ndugu Evaristo Ngalowaka, aliongoza maadhimisho hayo kwa kusisitiza umuhimu wa kuwekeza katika vyakula vyenye virutubisho sahihi ili kujenga jamii yenye afya bora na nguvu kazi imara.
Maadhimisho haya yaliakisi dhamira ya Halmashauri ya kuhakikisha kuwa kila mwananchi anapata elimu na uelewa wa kutosha juu ya umuhimu wa lishe bora. Katika hotuba yake, ndugu Evaristo aliipongeza Halmashauri kwa juhudi zake za kuimarisha afya ya jamii kwa kutoa elimu ya lishe hadi maeneo ya pembezoni.
Alieleza kuwa mpango huu wa elimu unaendeshwa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa afya na maendeleo, ikiwa ni moja ya mikakati ya Halmashauri kuzuia magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama kisukari na shinikizo la damu, ambayo yanachochewa na utumiaji wa vyakula vyenye mafuta na sukari nyingi.
“Tunajivunia kuona Halmashauri yetu inachukua hatua madhubuti za kutoa elimu ya lishe bora kwa wananchi wetu wote, hasa vijijini ambako uelewa kuhusu lishe bado ni changamoto. Tunataka kuhakikisha kuwa kila mwananchi anajua umuhimu wa lishe bora kwa afya ya mwili na maendeleo ya kiuchumi,” alisema ndugu Evaristo
Aidha, ndugu Evaristo alisisitiza kuwa lishe bora ina mchango mkubwa katika kuimarisha nguvu kazi ya taifa na kupunguza gharama za matibabu. Aliitaja jamii yenye afya bora kuwa ndiyo msingi wa maendeleo ya taifa.
Kwa kuhitimisha, ndugu Evaristo aliwasihi wananchi kuwa mabalozi wa lishe bora katika jamii zao. Alisema, “Halmashauri yetu itaendelea kusimama na nyinyi ili kufanikisha malengo ya kuwa na jamii yenye afya njema. Tunawaomba nanyi mshiriki nasi kwa kutoa elimu kwa familia na majirani zenu ili vizazi vijavyo vipate afya bora na nguvu kazi yetu iweze kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya nchi yetu.” Maadhimisho haya yamebeba kauli mbiu isemayo "Mchongo ni Afya Yako Zingatia Unacho Kula"
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa