Mkuu wa Wilaya ya Songea, Mhe. Kapenjama Ndile, ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Songea kwa usimamizi mzuri na uadilifu katika utoaji wa mikopo ya asilimia 10 kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, kama ilivyoelekezwa na Serikali.

Akizungumza wakati wa hafla ya utoaji wa mikopo hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa Jenista Mhagama uliopo Shule ya Sekondari Maposeni, Mhe. Ndile alisema amefurahishwa na namna Halmashauri ya Wilaya ya Songea inavyotekeleza agizo la Serikali kwa ufanisi mkubwa chini ya uongozi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri, Bi. Elizabeth Gumbo.
“Tunapokuwa na watendaji makini wanaojua wajibu wao na wanaojali wananchi, utekelezaji wa mipango ya Serikali huwa rahisi hongera sana Mkurugenzi na timu yako kwa kusimamia vema mchakato huu muhimu kwa maendeleo ya jamii yetu,” alisema Mhe. Ndile.
Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya alisisitiza umuhimu wa vikundi vinavyonufaika na mikopo hiyo kuhakikisha wanazitumia kwa malengo yaliyokusudiwa na kuzirudisha kwa wakati, ili kutoa nafasi kwa vikundi vingine kufaidika.
“Fedha ina uwezo wa kubadili maisha ya mtu, lakini pia inaweza kukupotosha iwapo hutakuwa makini, nawasihi muwe waangalifu msije mkatumia fedha hizi kwa matumizi yasiyo ya lazima na mkasahau malengo yenu,” aliongeza.
Awali, akifungua hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea, Bi. Elizabeth Gumbo, alisema kuwa zoezi hilo ni muendelezo wa utoaji wa mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri ambapo zaidi ya shilingi milioni 247 zimetolewa kwa vikundi 28 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Kwa upande wao, wanufaika wa mikopo hiyo walieleza furaha yao na kuishukuru Halmashauri kwa fursa waliyoipata. Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Stumai Willo alisema mikopo hiyo itawasaidia kukuza mitaji ya shughuli zao za kiuchumi na kupunguza utegemezi katika familia.
“Tunashukuru sana Halmashauri kwa kutuamini na kutuwezesha. Pia tunamshukuru Mbunge wetu Mhe. Jenista Mhagama na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuona umuhimu wa makundi maalum,” alisema Stumai.
Mikopo hiyo ni utekelezaji wa agizo la Serikali linalozitaka Halmashauri kutenga asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa ajili ya kuwawezesha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kiuchumi.
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa